Kama viongozi wetu walivyopata kutueleza, ili tuweze kupata maendeleo, ni lazima kuwepo na vitu vitatu: Ardhi, Uongozi Bora na Siasa Safi. Tayari vitu hivi vipo kwa sababu taifa letu linaendeshwa kwa misingi ya demokrasia, na ardhi ipo ya kutosha.
Hata hivyo, ni lazima kutambua kwamba, ardhi ama udongo ndiyo rasilimali mama ulimwenguni. Madini ya thamani yanapatikana ardhini, miti ya mbao inapatikana ardhini pamoja na mimea ya kila aina, bila kusahau kwamba viumbe hai wengine, binadamu na hayawani wa mwituni, nao pia wanaitegemea ardhi kwa ajili ya ustawi wao, kwani udongo huu unatumika kuzalisha kitu chochote ambacho kinahitajika kwa matumizi ya binadamu na wanyama.
Tumeirithi ardhi kutoka kwa vizazi vilivyotangulia ikiwa na ubora wa asili, lakini kutokana na matumizi ya muda mrefu, ardhi hii huzeeka na kushindwa kutoa mazao bora juu yake, hivyo kumfanya binadamu kutafuta namna nyingine ya kuifanya ardhi hiyo itoe mazao bora.
Katika sehemu kubwa ya nchi yetu, ardhi imekuwa chanzo cha migogoro ya mara kwa mara kutokana na matumizi yake, ambapo jamii za wakulima na wafugaji zimekuwa zikigombana – na hata wakati mwingine kusababisha maafa – kila moja ikisema inastahili kutumia ardhi hii.
Hii ni kwa sababu mkulima, baada ya kuona ardhi yake imechoka huamua kutafuta maeneo mengine yaliyo bora na kuanza kuyatumia. Wakati mwingine hulazimika kufyeka misitu ili kupata mashamba mapya, hali ambayo siyo tu inaharibu mazingira, lakini pia inaweza kututia umaskini wa milele kwa sababu ardhi iliyoachwa awali huwa haitafutiwi njia muafaka ya kuifanya irejee kwenye ubora wake.
Katika baadhi ya maeneo, wakulima wengine hutafuta mbolea, hasa za chumvi chumvi, na kuzitumia katika ardhi ile inayoonekana kuzeeka. Lakini matatizo mengi huibuka kutokana na matumizi ya mbolea pamoja na madawa ya kemikali kwenye kilimo. Hii ni kwa sababu mbolea hizi zina kemikali na yale madawa ya kuua wadudu yana madhara yake kwani yana sumu isiyoonekana. Hii sumu tunakula au tunakunywa na ndizo zinazoleta madhara kwa binadamu na udongo.
Aidha, mazao yatokanayo na kilimo cha mbolea hizi za kemikali yanaleta athari kubwa zisizoonekana kwa binadamu na hata wanyama. Lakini jambo la kuzingatia kwa sasa, kila mtu anatakiwa kuvuta kumbukumbu zake kulingana na umri alioishi na kuangalia yafuatayo:
Hali ya udongo enzi zile na sasa ikoje?
Kiwango cha maradhi wakati ule na sasa kikoje?
Uwezo wa udongo kuzalisha mazao umepungua au unazidi mwaka hadi mwaka?
Wengi wetu tumegundua kwamba mbolea za chumvichumvi zimechakaza udongo na hivyo kufanya uzalishaji upungue.
Hata mazao yatokanayo na matumizi ya mbolea hizo yamekosa ubora wa asili unaotakiwa.
Hii inatia shaka kama umaskini wa mkulima utakwisha ikiwa hatabadili aina ya pembejeo kuokoa ardhi yake isizidi kuchakaa, na wakati huo huo kupunguza sumu isiyoonekana kwenye udongo na vyanzo vya maji.
Katika mataifa mengi ya ulimwengu wa kwanza, mbolea za chumvi chumvi zinatumika kupandia na kukuzia miti, hasa ya mbao. Vile vile inatumika kutengenezea mazingira kwa maeneo ambayo hayatumiki kuzalisha mazao ya chakula cha binadamu.
Wao wamekuwa wakipiga sana vita vyakula vilivyolimwa kwa kutumia mbolea za chumvi chumvi, na ndiyo maana hivi sasa katika soko la dunia, bidhaa zilizozalishwa kwa kutumia mbolea hizi za chumvi chumvi zimekuwa zikiuzwa kwa bei ya chini kuliko zile zinazolimwa kwa kutumia kilimo hai.
Sasa tujiulize, kwa nini sisi tunaendelea kutumia mbolea hizi zinazoua udongo wetu na kuweka sumu?
Hivi hakuna mbolea nyingine mbadala?
Jibu ni kwamba, mbolea mbadala zipo.
MBOLEA MBADALA
Mbolea mbadala ni zile zinazotokana na marejea na uozo wa asili. Uozo wa asili unaotokana na majani mbalimbali, samadi ya mifugo asili; mabaki ya nafaka au mazao mbalimbali (kama maganda ya karanga, mabua ya mahindi, n.k.).
Mbolea hizi zinaweza kupatikana au kutengenezwa katika mazao tunayolima, kwenye mazingira tunayoishi. Mbolea hizi zinasaidia kurudisha udongo katika hali ya rutuba na asili yake na gharama za mbolea hizi ni nafuu kabisa na zinadumu ardhini kwa muda mrefu.
ZINGATIA
Jambo la kuzingatia ni kwamba, udongo ni mali pekee yenye thamani kubwa ambayo tumepewa na Mwenyezi Mungu. Hivi sasa kuna migogoro mingi vijijini kutokana na watu kukimbilia mashamba mapya kwa ajili ya kutafuta rutuba baada ya mashamba yao ya zamani kufa kutokana na matumizi ya mbolea zenye kemikali.
Ni ukweli usiopingika kwamba, mbolea za chumvi chumvi zikiisha muda wake hugeuka sumu na baadaye mkulima analazimika kutumia gharama kubwa kuweka mbolea za mboji ili kurudisha udongo katika hali nzuri. Sumu hii isiyoonekana inaharibu udongo, vyanzo vya maji na hata mwili wako mwenyewe.
Mkulima anahitaji kupata mazao bora na ya kutosha ili yamsaidie kwa chakula, na ziada inayopatikana auze kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya familia, lengo ambalo linaonekana kuwa gumu kufikiwa katika nyakati za sasa ambapo pembejeo za kilimo zimekuwa ghali na zaidi matumizi ya mbolea za kemikali yanazidi kuua ardhi, hivyo kupunguza uzalishaji wenyewe.
Aidha, hata mazao yatokanayo na kilimo cha mbolea za kemikali nayo hayana bei kubwa katika soko la dunia ikilinganishwa na mazao yatokanayo na kilimo hai, ambacho kwa sasa ndicho kinachohamasishwa ulimwenguni kwa sababu kinatumia viuatilifu asilia ambavyo siyo tu vinaongeza tija ya mazao, lakini pia ni rafiki wa mazingira.
Kwa mfano, katika mwaka 2003/2004 wastani wa bei za mazao ya kilimo hai ilikuwa takriban asilimia 20 hadi 50 juu ya bei za mazao yasiyo ya kilimo hai katika Soko la Jumuiya ya Ulaya na Marekani. Kwa mwaka 2005/2006 kahawa iliyozalishwa kwa kilimo hai (organic coffee) iliuzwa kwa Dola za Kimarekani (USD) 65.7 kwa kilo 50 ikilinganishwa na USD 50.0 kwa kilo 50 za kahawa iliyozalishwa kwa kutumia kemikali za kilimo (agro-chemicals). Aidha, vanilla iliyouzwa nchi za Jumuiya ya Ulaya ilipata premium ya asilimia 20 hadi 300.
Kilimo hai au organic farming ni aina ya kilimo kinachozingatia matumizi endelevu ya rasilimali za uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo. Kilimo hicho kinatumia mbolea na madawa yasiyotengenezwa viwandani na kinazingatia utunzaji wa mazingira kwa ajili ya manufaa kwa jamii, kiuchumi na kiafya.
Ili bidhaa zikubalike katika Soko la Kimataifa kuwa zimezalishwa kwa kutumia mbinu za kilimo hai, zinapaswa kwanza kupitishwa na Taasisi zinazosimamia ubora wa bidhaa hizo. Taasisi hizo ni International Federation of Organic Agriculture Movement (IFOAM) na Shirika la Ubora wa Viwango vya Vyakula la Umoja wa Mataifa (Codeaux Alimentarius Commission). Soko la mazao ya kilimo hai hutegemea walaji wa mazao hayo ambao wapo tayari kulipa bei kubwa kwa mazao ambayo yamezalishwa bila ya kutumia viatilifu na mbolea za viwandani.
Kilimo hai nchini kilianza kupata umaarufu katika miaka ya 1990 baada ya Serikali kuruhusu Taasisi kadhaa zisizo za Kiserikali (NGO) zikiwemo EGAJ, INADESTZ, PELUM, Meatu Cotton Projects, Babati LAMP na nyinginezo zilizojitokeza kueneza elimu na teknolojia za kilimo hai.
Aidha, Serikali kwa kutambua umuhimu wa kilimo hai na nia ya kuwasaidia wakulima kuendeleza kilimo hicho imeweka vipengele muhimu kwenye sera yake ya kilimo ikiwa ni pamoja na kuruhusu Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kusimamia biashara na bidhaa zake ambapo mwaka 2005 iliruhusu kuundwa kwa Tanzania Organic Agriculture Movement (TOAM) yenye lengo la kuwaunganisha wadau wa kilimo hai na kuwajengea uwezo.
Kutokana na juhudi hizo hivi sasa kilimo hai kinalimwa katika Mikoa ya Kilimanjaro, Tanga, Kigoma, Iringa, Pwani, Kagera, Mbeya, Morogoro, Shinyanga na Arusha. Mazao yanayozalishwa kwa njia ya mkataba ni pamoja na kahawa, chai, korosho, cocoa na pamba. Mazao mengine ni matunda na viungo hususan mananasi, tangawizi, tumeric, vanilla, pilipili na vitunguu. Sehemu kubwa ya bidhaa wanazozalisha zinauzwa moja kwa moja katika Soko la Jumuiya ya Ulaya na kiasi kidogo katika Soko la Marekani.
Hata hivyo, masharti yanayoambatana na kilimo hai yanakuwa magumu kwa baadhi ya wakulima na hivyo wakulima wengi kushindwa kuzalisha mazao hayo pamoja na kuwa yana bei kubwa.
Utafiti wa kina unafanywa na Mashirika ya Nchi za Afrika Mashariki ambayo ni Kenya Organic Agricultural Network (KOAN), National Organic Agricultural Movement of Uganda (NGAMU) na Tanzania Organic Agricultural Movement (TOAM) ili kuboresha uzalishaji na fursa za biashara ya bidhaa za kilimo hai katika nchi za Afrika Mashariki. Matokeo yatatolewa baada ya utafiti kukamilika.
Kilimo hai ni muhimu sana nchini Tanzania na mkombozi wa mkulima kwa kuwa kitamfanya kudumu mahali pamoja kwa muda mrefu na kuweza kujipanga vyema namna ya kujikwamua kimaisha. Pia kilimo hai kitainusuru nchi isigeuke jangwa kutokana na watu wanaokimbilia kufyeka misitu kwa minajiri ya kutafuta ardhi yenye rutuba, na zaidi kitasaidia kupunguza migogoro baina ya wakulima na wafugaji ambayo inatokea sasa.
Mikakati ya kuhamaisha kilimo hai ni elimu ya uhamasishaji ambayo inatakiwa ianzie ngazi ya chini, kwa mkulima mmoja mmoja, kwa vikundi tukitumia viongozi wa vijiji, kata, wilaya, mikoa na taifa ili kila mtu afahamu faida zake kwa ukamilifu.
Uwepo wa pembejeo za mboji nchini utamkwe kwa wananchi na serikali yenyewe. Hii itasaidia wakulima waelewe haraka na itasaidia kuharakisha watu wanaotaka kuweka miradi ya kutengeneza pembejeo hizo hapa nchini wapate mwelekeo mzuri.
Pembejeo za mboji pia zinapaswa kutambuliwa na kuingizwa kwenye ruzuku kama pembejeo zingine ili mkulima apate unafuu na serikali haipaswi kupendelea zaidi mbolea za kemikali.
Serikali inatakiwa kuongeza juhudi zaidi katika kuhamasisha wananchi waendeleze kilimo hai, ambacho ni endelevu na rafiki wa mazingira, ili kiwanufaishe zaidi kwani mazao yatokanayo na kilimo hicho yana uhakika wa soko ulimwenguni tofauti nay ale yanayotumia mbolea za kemikali.
Kukaa kimya kwa serikali kunamaanisha kwamba hata wadau wanaojitokeza kushabikia kilimo hai nchini watakata tamaa, kwani hata mbolea asilia wanazoziagiza kutoka nje ama kuzitengeneza zinakosa soko kutokana na wakulima kutokuwa na elimu na maafisa kilimo kugoma kuhamasisha utumiaji wa mbolea hizo kwa maelezo kwamba hawajapewa maagizo kutoka wizarani.
Kama kweli tunataka kujikomboa kupitia kilimo, kwa kweli hatuna budi kutumia zaidi kilimo hai ambacho pia kinaweza kutuepusha na migogoro ya ardhi kama inayojitokeza sasa baina ya wakulima na wafugaj