MKUU WA MKOA WA NJOMBE ATAKA TRA NA TFDA WASHIRIKIANE AKIWA KATIKA ZIARA YA KUTEMBELEA MABANDA YA NANE NANE MBEYA.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe Kepten Mstaafu Aseri Msangi akipata maelezo mbali mbali katika Banda la Tanseed.
Kaimu Meneja wa TFDA Kanda ya Nyanda za juu kusini Rodney Alananga akimuonesha Mkuu wa Mkoa baadhi ya bidhaa feki ambazo hazifai kwa matumizi ya binadamu.
Mkuu wa Mkoa akiangalia kiroba cha Konyagi kilichobandikwa nembo feki ya TRA.
Afisa elimu kwa Mlipa kodi (TRA)wa Mkoa wa Iringa, Masunga Faustine akikichunguza kwa makini kiroba cha Konyagi ili kuangalia namna ilivyochakachuliwa.
Maafisa wa TRA wakifafanua jambo kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa.
***************
MKUU wa Mkoa wa Njombe, Kepteni Mstaafu Aseri Msangi, ameziagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya udhibiti wa chakula na dawa(TFDA) kuwa na mahusiano ya karibu.
Agizo hilo alilitoa jana katika ziara ya kutembelea mabanda ya maonesho ya wakulima nanenane yanayoendelea katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.
Msangi alisema kukiwa na mahusiano mazuri baina ya mamlaka hizo mbili kutachangia kudhibiti uingiaji na matumizi ya bidhaa feki hapa nchini.
Aidha alilazimika kutoa agizo hilo baada ya Tfda kubaini matumizi ya nembo ya TRA katika vinywaji vikali vinavyozalishwa na Konyagi kutumika katika pombe feki.
Katika ziara hiyo ambayo Mkuu wa Mkoa huyo alipitia mabanda ya Tra na Tfda alibaini kutokuwa na mahusiano na ushirikiano kutokana na Afisa wa Tra kushindwa kuigundua nembo yao kama ni Feki.
Akifafanua mbele ya Mkuu wa Mkoa kuhusu pombe feki, Kaimu Meneja wa TFDA kanda ya Nyanda za juu kusini, Rodney Alananga, alisema mbali na Serikali kupiga marufuku uingizwaji na matumizi ya Pombe kali kutoka nje ya nchi lakini pia imegundulika kuchakachuliwa kwa pombe za ndani.
Alananga alitolea mfano ni pombe aina ya Konyagi inayozalishwa na kampuni ya Tanzania Distillers Limited(TDL)kuwa wafanyabiashara wanafoji nembo ya TRA inayopaswa kubandikwa kwenye chupa na karatasi la kinywaji hicho.
Alizitaja baadhi ya sifa zilizokutwa katika pombe iliyochakachuliwa kuwa ni pamoja na utoafuti wa ujazo ulioandikwa kwenye nembo ya TRA na Nembo ya Kiwanda ambapo Kiwanda kimeandika ujazo wa ml 100 na kwenye nembo ikisomeka Ml 10.
Tofauti zingine ni pamoja na kutofautiana kwa jina la kiwanda, jina la bidhaa na biashara kukosekana kwa tarehe ya kuanza kutumika na mwisho wake pamoja na nembo hiyo feki kufutika kirahisi kuliko nembo halisi.
Kwa upande wake Afisa Elimu kwa Mlipa Kodi Mkoa wa Iringa, Faustin Masunga, alikiri kutojua tofauti hizo na kuahidi kuzidi kutoa elimu kwa wananchi ili kuepuka kuhatarisha afya za watu.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Kapt Mstaafu Aseri Msangi aliiagiza Mamlaka ya mapato (TRA) kujikita katika uoaji wa elimu kwa wanunuzi na walaji ili kuongeza ukusanyaji wa mapato.
Alisema endapo mnunuzi ataelimishwa juu ya sheria ya kodi(EFD Regulation ya Mwaka 2010) ya kumtaka anaponunua kitu adai risiti itasaidia kuongeza kwa ukusanyaji wa mapato nchini.
Alisema katika utoaji wa elimu wanapaswa kufuata mfumo wa Serikali ambao hutaka kumshirikisha kuanzia ngazi ya kijiji hadi ngazi za juu ambao ndiyo wenye watu na wanaopaswa kukusanya watu endapo watataka kutoa elimu.
Katika ziara hiyo Mkuu huyo wa Mkoa pia alitembelea mabanda ya kuzalisha mbegu ya Tanseed, Bodi ya Pareto,Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe, Mamlaka ya hali ya hewa na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.
by; kilimo tija