Sunday, 21 April 2013

Kukauka Mto Ruaha Mkuu, Mbarali lawamani


Wakazi wa kata za Igoma na Ilungu wilayani Mbeya vijijini wamelalamikia matumizi yasiyo sahihi ya maji kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo cha umwagiliaji katika wilaya ya Mbarali na kudai kuwa shughuli hizo zinachangia kwa kiasi kikubwa kukausha mto Ruaha Mkuu ambao ndiyo uhai mkuu wa hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Wamesema katika kata zao ambazo zipo katika milima ya Livingstone wamekuwa wakifanya juhudi kubwa kuhifadhi vyanzo vya maji ili kuitikia wito wa Serikali na wadau wengine wa kuokoa Hifadhi ya Ruaha na bwawa la Mtera lakini maji mengi yamekuwa yakipotelea katika wilaya ya Mbarali huku TANAPA na mamlaka zingine wakifumbia macho suala hilo.
Ndani ya hifadhi ya Taifa ya Ruaha, uoto wa asili hivi sasa unapendeza kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha lakini mto wa Ruaha Mkuu hali yake bado si ya kuridhisha angalau maji sasa yanatiririka baada ya kutofanya hivyo kwa takribani miezi minne iliyopita.
Hali hii inawashtua wananchi wanaotoka kwenye vyanzo vya maji yanaoingia Ihefu na hatimaye mto Ruaha Mkuu walioongozana na Mkuu wa wilaya ya Mbeya vijijini kwa ajili ya ziara ya mafunzo ndani ya hifadhi ya Ruaha ambao wanasema juhudi kubwa wanazofanya kuhifadhi vyanzo vya maji zinaishia wilaya ya Mbarali.
Wakizungumza katika kikao cha majadiliano baada ziara yao, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya mbeya vijijini Bi. Upendo Sanga na Mkuu wa wilaya hiyo Dokta Norman Sigalla wamesema ni vyema kuwa na kikao cha pamoja kujadili jambo hilo na kuwa na utaratibu usiochekea watu wanaotumia maji kiholela hususani wanaolima kilimo cha umwagiliani bila miundombinu ya kurejesha maji mtoni
Akijibu hoja hizo, Afisa Utalii mwandamizi wa hifadhi ya Taifa ya Ruaha Bi. Eva Pwelle amesema siyo kweli kwamba TANAPA imekuwa haishughulikii tatizo hilo na hivi sasa kwa kushirikiana na wadau wengine imekuja na mradi wa kuimarisha usimamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa kusini mwa Tanzania (SPANEST) ambao pia utashughulikia tatizo hilo.
Uongozi wa juu wa wilaya ya Mbeya vijijini pamoja na kamati za maendeleo za kata za Igoma na Ilungu na wazee maarufu wa kata hizo  wametembela hifadhi ya Taifa ya Ruaha kujifunza umuhimu wa uhifadhi kwa ufadhili wa Mradi wa SPANEST.

No comments:

Post a Comment